Joto la kampeni laongezeka Monduli, Ukonga

Joto la kampeni laongezeka Monduli, Ukonga

12 September 2018 Wednesday 10:07
Joto la kampeni laongezeka Monduli, Ukonga

Mambo yote ni Jumapili. Ni siku ambayo utafanyika uchaguzi mdogo katika majimbo mawili la Monduli, Ukonga na kata nyingine 22 nchini.

Katika siku hizo za lala salama hamasa na nguvu ya kampeni inazidi kuongezeka kwa kila upande, hasa vyama viwili vyenye ushindani mkubwa nchini CCM na Chadema.

Tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imewaalika waangalizi wa ndani wa uchaguzi kushuhudia mtanange huo katika sanduku la kura.

Vyama hivi vimeamua kuacha kazi na kufanya kazi. Vinahakikisha vigogo wake na wagombea wanapita kila kona ya majimbo yao kunadi sera na kutoa ahadi mbalimbali za kuleta maendeleo na mikopo kwa akinamama na vijana.

Mbali na wabunge kutoka katika vyama vya CCM na Chadema, wapo viongozi wakuu wa vyama na mawaziri hasa kwa chama tawala ambao wanajitahidi kumwaga sera na ahadi mbalimbali.

Jimbo la Ukonga

Katika maeneo mengi kwenye jimbo la Ukonga vyama vitatu CCM, Chadema na CUF vimeonekana kunyang’anyana wananchi wa kusikiliza hoja zao kwenye kampeni hizo.

Maeneo mengi ambako kuna mikutano ya kampeni, wananchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kusikiliza na kushangilia kila mgombea au kiongozi wa chama husika anapohutubia.

Wiki moja nyuma, hali ilikuwa tofauti na sasa, vyama hivyo vilikuwa vikifanya mkutano mmoja, kwa siku lakini sasa vinafanya zaidi ya mmoja.

Vyama hivyo vinavyopishana katika kila kata za jimbo hilo. Shughuli sasa imekuwa kubwa, wagombea na wapambe wao wanabadilishana viwanja vya kampeni. Akitoka huyu asubuhi mwingine anaingia mchana au jioni, kama siyo siku inayofuata ili kufuta nyayo.

Akizungumzia mchakamchaka huo, mgombea wa ubunge kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara anasema anafanya mikutano mitatu hadi mitano kwa siku, ikiwamo ya kukutana na wananchi kwenye mikutano midogomidogo ya kata kuanzia saa 4:00 asubuhi.

“Mikutano mikubwa tunafanya miwili kuanzia saa 8:00 mchana hadi saa 12:00 jioni,” anasema.

Waitara ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo akajiuzulu na kugombea tena, anaeleza kuwa lengo la kuongeza kasi ya kufanya mikutano katika wiki ya mwisho ni kuhakikisha anazimaliza kata za jimbo hilo. Jimbo hilo lina mitaa 70 na kata 13.

“Unajua yamesemwa maneno mengi kuhusu kuhama kwangu, sasa nataka nifike kwenye kila mtaa na kila kata kuhakikisha naondoa uongo walioueneza dhidi yangu,” anasema Waitara.

Anasema kuwa hadi sasa mwitikio wa mikutano unakwenda vizuri.

Anafafanua kuwa uwezo wa kufanya hivyo anao na nia ya kuwa mbunge wa wana-Ukonga anayo, ndiyo maana hatabakisha eneo ambalo hajafika kuzungumza na wananchi.

“Nataka pia wajue kwa nini nimeamua kupitia chama kingine. Wameshatambua kuwa wagombea kutoka vyama vingine kikiwamo Chadema ni wasindikizaji, hivyo wamejipanga kunipa jimbo,” anasema Waitara.

Mchakamchaka wake

Katibu wa CCM Ilala, Joyce Mkangale anasema tangu kampeni zilipoanza kila siku wanafanya mikutano miwili.

Anasema wanagawa muda, wanaanza kufanya mkutano wa kwanza saa 8:00 mchana hadi saa 9:00 alasiri na mkutano wa pili huanza saa 10:00 jioni hadi saa 12:00 jioni.

“Kwa mwitikio ulivyo tuna uhakika wa kushinda, mikutano yote watu wanajaa na wana hamasa ya kuendelea kufanya kazi na jembe lao Waitara,” anasema Mkangale.

Ukiacha mikutano ya moja kwa moja ya kampeni pia kuna miradi ya kiserikali inayohamasishwa kipindi hiki kama umeme wa Rea, na utatuzi wa migogoro ya ardhi yenye harufu ya kampeni.

Safari ya CUF

Kaimu mwenyekiti wa CUF wilaya ya Ilala, Hamisi Chambuso anasema kwa siku wanafanya mikutano miwili.

Anasema kwa jimbo wanafanya mkutano mmoja na mwingine katika Kata ya Vingunguti ambako pia wamesimamisha mgombea.

Chambuso anasema kabla ya kufanya tathmini ya pamoja kwa kuangalia hali ya mikutano ni nzuri na mwitikio kwa wananchi ni wa kuridhisha.

“Ukipata wananchi kwenye maeneo ya pembezoni na wakajaa kusikiliza sera zako, ujue wamehamasika,” anasema.

Hata hivyo, mgombea wa jimbo hilo kupitia CUF, Salama Masoud anasema kufanya mikutano mingi si hoja, hoja ni namna ambavyo wananchi wanaowafikia wanaelewa nia na lengo lake la kuwatumikia.

Anasema wanajitahidi kwa kila hali kuhakikisha wanafika maeneo ya mbali kunadi sera na dhana nzima ya kuomba ridhaa ya kuwaongoza.

“Kutokana na uimara wa sera zetu, bila shaka wananchi wa jimbo la Ukonga anapeana habari na kuzitafakari kabla ya kunipa ridhaa ya kuwaongoza Septemba 16,” anasema Masudi.

Mbio za Chadema

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema anasema kwao kampeni ndiyo kila kitu katika wakati huu wa lala salama.

“Katika kuhitimisha kampeni zetu za Ukonga na Monduli wiki hii ya mwisho yapo mambo ambayo yatafanyika ikiwa ni pamoja na viongozi wakuu wakiongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe kuungana kuwanadi wagombea.

“Wabunge na viongozi mbalimbali wa chama wamekuwa wakifanya kazi hiyo na katika kuhitimisha nguvu itakuwa kubwa zaidi,” anasema Mrema.

Anasema badala ya kufanya mikutano miwili, watakuwa wanafanya minne katika majimbo yote.

Anasema mwitikio wa wananchi unadhihirisha kuwa kuna kitu wanakitaka na wanaamini watakipata kwa mgombea wa Chadema.

Mzunguko wa Asia Msangi

“Kote ninakopita nawasisitiza wananchi malengo na mipango nitakayofanya pamoja nao iwapo watanipa ridhaa ya kuongoza jimbo hili.

“Ninajua wengi wanataka mabadiliko na wanajua Asia Msangi ndiyo mwenye sifa ya kuwapa, ninawaomba wajitokeze kwa wingi Septemba 16 kupiga kura ya ndiyo kwangu,” anasema Msangi.

Yanayojiri Monduli

Kama ilivyo Ukonga, katika wiki ya mwisho ya kampeni katika Jimbo la Monduli, vyama vinane pia vimeongeza kasi ya kampeni kwa kufanya mikutano zaidi ya miwili kwa siku.

Miongoni mwa vyama vyenye upinzani mkubwa jimbo la Monduli ni CCM na Chadema, ambavyo wagombea wake, Julius Kalanga (CCM) na Yonas Laizer (Chadema) wanatoka katika kata moja ya Lepurko.

Kujitokeza kwenye kampeni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo, Waziri wa Nishati, Medard Kalemani na naibu mawaziri kadhaa kumeongeza sana nguvu ya CCM kwenye kampeni.

Mawaziri hao licha ya kujibu kero mbalimbali, baadhi walitoa ufumbuzi wake na hivyo kujihakikishia kuungwa mkono kwa mgombea wa CCM, Julius Kalanga.

Kampeni za CCM

Meneja kampeni za CCM, William Ole Nasha, anasema wiki ya mwisho ya kampeni ameongoza idadi ya mikutano, lakini pia anawatumia wabunge wa chama hicho zaidi ya 12 na mawaziri kujibu kero za wananchi.

“Tumejipanga vizuri, tuna kampeni kila kata, kwani Monduli ina kata 20 na kule tuna kampeni ikiwepo waratibu wa kata, ndio sababu tuna uhakika wa ushindi,” anasema.

Alisema katika kampeni, wamekuwa wakitatua kero za wananchi na kutoa ahadi tofauti na vyama vingine ambavyo vinaomba kura za ‘heshima’.

Chadema chini ya Lowassa

Kampeni za Chadema ambazo zinaongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa zimekuwa za kasi pia, kwani licha ya kufanyika mikutano ya hadhara kumekuwapo na mikutano ya ndani na nyumba kwa nyumba na kwenye minada.

Akizungumza na wananchi wa Kata za Makuyuni, Mto wa Mbu na Meserani, Lowassa aliwahakikisha wananchi ushindi na kuwataka wajitokeze kupiga kura.

Kama ilivyo kwa Waitara, Kalanga naye alijiuzulu ubunge kupitia Chadema na kuhamia CCM ambayo imemteua tena kuwania nafasi hiyo.

Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa alisema, Chadema sasa imejipanga kuongeza viongozi wa kitaifa na wabunge wake katika Jimbo la Monduli.

“Wiki ya mwisho tunaongeza nguvu, Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Vincenti Mashinji, Naibu katibu mkuu Zanzibar, Salimu Mwalimu na wabunge watakuja Monduli,” alisema.

Meneja kampeni ya Chadema, Patrick Ole Sosopi, aliwataka wananchi kupuuza kauli kuwa, hata kama wakichaguliwa Chadema, matokeo hayatatangazwa wameshinda.

“Nyie jitokezeni kupiga kura kwa wingi na kulinda kura zetu, mambo mengi mtuachie sisi kwani tumejipanga kutetea ushindi wetu,” alisema

Vyama vingine vya upinzani, ACT- Wazalendo, AAFP, Tadea, DP, NRA na Demokrasia Makini ambavyo kampeni zake zimekuwa zikisuasua, wiki hii pia vimetangaza kuwashirikisha viongozi wake wa kitaifa.

Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo mkoa wa Arusha, Mwahija Choga, alisema viongozi wa kitaifa wa chama hicho, watafika Monduli kuongeza nguvu za kampeni.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.