Kamati kuu ACT wazalendo yaibuka na maazimio matano

Kamati kuu ACT wazalendo yaibuka na maazimio matano

11 June 2019 Tuesday 11:42
Kamati kuu ACT wazalendo yaibuka na maazimio matano


Na mwandishi wetu, Dar es Salaam
JUNI 9 na 10, 2019 kamati kuu ya  ACT Wazalendo ilikutana jijini Dar es salaam katika kikao  cha kawaida. Pamoja na mambo mengine imepitia  mwenendo wa hali ya kisiasa na kiuchumi nchini  na Bara la Afrika kwa ujumla na  imetoa maazimio yafuatayo;
 
1. Tunalaani Mauaji ya Raia Nchini Sudan
 
Chama cha ACT Wazalendo kinatoa salaam za mshikamano kwa waafrika wenzetu wa Sudan ambao wanapita kwenye wakati mgumu sana katika harakati za kupigania Demokrasia nchini kwao. Baada ya kufanikiwa kuangusha utawala wa kidikteta wa Rais Omar Al Bashir, Wananchi wa Sudan sasa wanakabiliwa na mtihani mzito wa kuhakikisha wanapata Serikali ya kiraia.
 
Hivi sasa kuna mauaji makubwa yanaendelea yanayofanywa na kundi la kijeshi lililopora mapinduzi ya mwananchi wa Sudan. Chama chetu kinalaani vikali mauaji haya na kuungana na tamko la Umoja wa Mataifa na lile la Umoja wa Afrika la kutaka Uchunguzi wa kina wa matukio ya mauaji huko Sudan.
 
Pia Kamati Kuu ya ACT Wazalendo imepitisha Azimio la kuitaka Serikali ya Tanzania, kwanza kulaani mauaji ya Wananchi wa Sudan, pili kuunga mkono maamuzi ya Umoja wa Afrika, na tatu kumhoji Balozi wa Sudan nchini Tanzania Kuhusu matendo ya mauaji ya raia wasio na hatia nchini Sudan.
 
2. Tutaimarisha Ushirikiano na Vyama Vyengine vya Upinzani Nchini
 
Kamati Kuu ya ACT Wazalendo imewapongeza viongozi wakuu wa chama kwa kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na vyama vingine vya siasa katika kuipigania, kuitetea na kuilinda misingi ya kidemokrasia nchini ambayo imevurugwa kwa kiasi kikubwa na Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano. Kamati Kuu imewaagiza viongozi wakuu wakuu wa chama kuendelea kushiriki kikamilifu kwenye ushirikiano na vyama vingine na pia kuhakikisha utekelezaji thabiti wa Azimio la Zanzibar lililoutangaza mwaka huu kuwa mwaka wa mapambano ya kudai demokrasia.
 
Pia, Kamati Kuu imemuagiza Katibu Mkuu wa Chama kuwaandikia makatibu wakuu wa vyama vyote tunavyoshirikiana navyo kuitisha kikao cha viongozi wakuu kutafakari namna bora ya vyama vya upinzani kushirikiana kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
 
3. Tutashiriki Kupigania Tume Huru na Uchaguzi Huru

Kwa uzito wa kipekee, Kamati Kuu imeendelea kuwapongeza Mwanaharakati Bob Chacha Wangwe na Wakili Fatma Karume kwa kusimamia vema kesi ambayo kwayo Mahakama Kuu ya Tanzania ilibatilisha vifungu kwenye sheria ya uchaguzi ambavyo vilikuwa vinawapa nafasi Wakurugenzi wa Halmashauri ambao wengi ni makada wa CCM kuwa wasimamizi wa uchaguzi. Chama chetu kitaendelea kuwaunga mkono Bob Chacha Wangwe na Wakili Fatma Karume katika kuhakikisha kuwa uamuzi wa mahakama unaheshimiwa.
 
Pia, Kamati kuu imewaagiza wanasheria wa chama kufungua kesi ya kikatiba chini ya hati ya dharura kuomba tafsiri ya kimahakama iwapo hukumu ya mahakama kuu kwenye kesi ya Bob Chacha Wangwe inaathiri ushiriki wa Wakurugenzi wa Halmashauri kama wasimamizi wa uchaguzi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
 
Kwa upande wa Zanzibar mabadiliko ya Sheria ya Uchaguzi yameipa ZEC mamlaka makubwa ya kuvuruga uchaguzi. Pia yameruhusu wanajeshi na watu wa usalama kupiga kura kabla ya siku ya uchaguzi jambo ambalo laweza kutumika vibaya na hivyo kuiba uchaguzi iwapo halitawekewa utaratibu bora na wa haki kwa wadau wa uchaguzi. Kamati Kuu imewapa maelekezo wanasheria wa chama kufungua mashtaka mahakamani ili kuondoa vifungu vipya vya Sheria ya Uchaguzi Zanzibar ambavyo ni hatari kwa uchaguzi huru na haki.
 
4. Hali ya Uchumi Ni Mbaya
 
Kama ilivyo ada, Kamati Kuu ilipokea na kuijadili ripoti juu ya hali ya uchumi wa nchi ambayo ilionyesha dhahiri kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wetu imeporomoka sana kwa sababu Serikali ya CCM ya Awamu ya 5 chini Rais John Magufuli inakata nishati ya kuendesha uchumi wetu (mauzo nje, wafadhili na uwekezaji mitaji-FDI)
 
Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania zinaonyesha kuwa kwa Mwaka unaoishia Machi 2018 urari wa Biashara kati ya Tanzania na nchi nyengine duniani ulikuwa hasi kwa USD 2 Bilioni. Kwa mwezi unaoishia Machi 2019 urari wa Biashara umetanuka kufikia hasi ya USD 2.5 Bilioni sawa na ongezeko la USD 500 milioni. Hii ni Kwa sababu mauzo nje ya bidhaa za Tanzania yameshuka. Mfano dhahiri ni Korosho mwaka 2018 (Tanzania imepoteza USD milioni 500), Mbaazi mwaka 2017 (Tanzania imepoteza USD milioni 250), Bidhaa za Viwanda 2017 na 2018 (Rais Magufuli alipokea kijiti Cha Urais Tanzania ikiwa inauza Bidhaa za Viwanda Nje za thamani ya USD Bilioni 1.3, sasa hivi tunauza USD milioni 872 tu).  
Urari wa Malipo ya Bidhaa na Huduma umeongezeka mpaka nakisi ya USD milioni 655 mpaka Machi 2019. Mwaka unaoishia Machi 2016, Urari wa malipo (overall balance of payments) ulikuwa na nakisi ya USD milioni 241 tu. Takwimu Hizi zinaonyesha kuwa nchi yetu inalipa zaidi nje Fedha za Kigeni kuliko inavyopokea na Kwamba uwezo wetu kwenye Biashara ya Nje umeshuka kwa 300% tangu Mwaka 2015. Kwa upande wa Zanzibar mauzo nje pia yameshuka na kuifanya Zanzibar kuwa na urari hasi wa Biashara (USD -50 milioni) mpaka Machi 2019 kutoka urari chanya (USD 37 milioni) mwezi Machi Mwaka 2018.
 
Nishati ya pili ya Uchumi ni misaada kutoka nje. Wafadhili wamezuia misaada na hivyo kuathiri utekelezaji wa Bajeti. Nchi mbalimbali zilizokuwa rafiki wa Tanzania zimezuia fedha za kigeni walizopanga kuipa Tanzania ili kutekeleza miradi mbalimbali. Hata taasisi kama Benki ya Dunia wamezuia Fedha kuja Tanzania. Fedha ambazo zimezuiliwa ni pamoja na ambazo zinapaswa kufadhili miradi ya kuboresha Elimu ya Sekondari SEQIP (USD 400m Sawa shilingi Bilioni 920) TASAF III (USD 300m Sawa na shilingi Bilioni 660) na Mradi wa Maji Vijijini (USD 300m Sawa na shilingi Bilioni 660).
 
Fedha hizi zimezuiwa Kwa sababu ya Serikali kutunga sheria kandamizi ya Takwimu kwa lengo la kuwadhibiti wakosoaji wa Serikali wanaotumia ushahidi wa takwimu Lakini madhara yake kwa nchi ni makubwa mno. Sababu nyingine Ni ubinywaji wa Demokrasia nchini, msingi wake Mkuu ukiwa ni kuporwa kwa ushindi wa Maalim Seif Sharif Hamad Katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2015. Kisha vitendo vya kuzuia Bunge Live, kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa vya Upinzani (ya CCM ikiruhusiwa), na kuwabambikia kesi mbalimbali wanasiasa wa upinzani, kupigwa risasi kwa Mbunge Tundu Lissu akiwa kwenye eneo la Bunge, na Kutungwa kwa sheria mpya ya vyama vya siasa inayoua kabisa siasa za vyama vingi nchi.
 
Nishati ya Tatu ya Uchumi ni Uwekezaji kutoka Nje. Kupungua kwa Uwekezaji nchini (FDI) kunapekelea shughuli za Uchumi kutoongezeka, kutozalisha ajira rasmi za kutosha na kutoongeza Mapato ya Serikali. Taarifa ya Benki ya Dunia (Economic Update No. 11) inaonyesha Kuwa Uwekezaji kwa uwiano wa Pato la Taifa (GDP) umeshuka kutoka 5% ya GDP mwaka 2015 mpaka 2% ya GDP mwaka 2018. Hii maana yake ni kuwa jumla ya shilingi Trilioni 4 zimeondoka kutoka Uchumi wetu Katika kipindi Cha miaka 3 tu.
 
5. Sekta Binafsi Inauliwa
 
Kwa Miaka 4 sasa Rais Magufuli na Serikali yake wamekuwa na msimamo madhubuti wa kuhakikisha sekta binafsi nchini inaanguka. Juzi tumeshuhudia Serikali ikianikwa na wafanyabiashara namna ambavyo utekelezaji wa sera za kodi umeua biashara na hata viwanda vingi kufungwa na watu wengi kupoteza ajira.

Baada ya Rais kutangaza kuwa alitaka wanaoishi kitajiri waishi kishetani, juzi tumeshuhudia akigeuka na kusema kuwa anataka kuacha Mabilionea 100 akimaliza muda wake. Tanzania ilikuwa imeshafika huko wakati anachukua utawala wa nchi yetu. Miaka 4 ya utawala wa Rais Magufuli imewashusha Watanzania waliokuwa wamefikishwa kwenye ubilionea tangu wakati wa mabadiliko ya kiuchumi yaliyofanywa na Rais Mkapa na kuendelezwa na Rais Kikwete kutoka ubilionea mpaka kuwa hohehahe.
 
Sera za Serikali ikiwemo kutolipa fedha halali kwa sekta binafsi kumepelekea watu kufilisika kabisa. Kwa mfano, Serikali inadaiwa na wenye viwanda jumla ya shilingi trilioni 2.3 za fedha za VAT refunds ambazo zimerundikana kwa miaka 3 Sasa. Hizi ni Fedha za Wafanyabiashara ambazo Serikali inapaswa kuwarudishia kufuatia malipo ya Kodi ya VAT. Serikali inaamua kuzipora na kuzitumia na hivyo kukosesha mtiririko mzuri wa fedha kwa viwanda (Cash flow problems), kushindwa kulipa mikopo kwenye mabenki na kuongezeka kwa gharama za Biashara. Sasa hata Rais akikutana na wafanyabiashara mara ngapi iwapo Serikali itaendelea kukwapua fedha za Wafanyabiashara inasaidia nini kuendesha Uchumi?
 
Mfano mwingine wa dhahiri wa kuchoka kwa serikali ya Rais Magufuli katika kuendesha uchumi wa nchi ni kuhusu suala la vitambulisho vya wajasiriamali. Fedha zinazokusanywa kupitia vitambulisho hivi ni kinyume na sheria inayotaka kila kodi kutamkwa na kuidhinishwa na Bunge. Mapato haya pia hayaonekani kwenye vitabu vya mapato ya serikali. Kukiuka taratibu za kodi tulizojiwekea wenyewe kunatoa mwanya kwa fedha hizi kutumika kwa matumizi haramu tofauti na matumizi halisi ya kodi ambayo ni kuwaletea mapato wananchi. Tuna hakika gani kwamba fedha hizi hazitaporwa na serikali ya CCM kama zilivyoporwa fedha za korosho, Escrow na EPA?
 
Utaratibu huu wa vitambulisho vya wajasiriamali ni mwendelezo wa kuzipora halmashauri zetu zenye dhamana ya kuendeleza huduma kwa wananchi vyanzo vyake vya mapato. Mathalani, Kwa Manispaa ya Kigoma Ujiji peke yake ambayo tunaiongoza, inakadiriwa kuwa Shilingi 281, 556, 000 za mapato ya ndani ya halmashauri zitapotezwa kutokana na vitambulisho vya wajasiriamali.
Tunarudia rai yetu kwa Rais John Magufuli kwamba akubali tu kuwa amesimamia uharibifu mkubwa wa uchumi wa nchi yetu na hivyo apishe watu wengine watakaoweza kurudisha uchumi wetu kwenye reli sahihi. Ni aibu kubwa kukabidhiwa nchi yenye uchumi unaokua kwa 7% kwa miaka 10 mfululizo halafu wewe ndani ya miaka 3 unaupeleka uchumi kwenye msinyao ( negative growth). Tunasisitiza rai yetu ya huko nyuma kuwa Rais Magufuli na Baraza lake la Mawaziri hawapaswi kuwa Ikulu bali wanapaswa kuwa kizimbani kujibu mashtaka ya uhujumu uchumi (economic sabotage).
 
6. Hitimisho
 
Tanzania inahitaji MABADILIKO, Watanzania wanahitaji MABADILIKO. Kwa kutumia matokeo ya Uchaguzi wa Mwaka 2015 Watanzania waliowengi (58%) waliamini kuwa mgombea wa Chama Tawala  anawakilisha mabadiliko na katika siku za mwanzo watu wengi tukaaminishwa kwamba kweli tunaelekea kwenye mabadiliko. Miaka 4 sasa nyinyi na sisi tumeona kwamba CCM ni ile ile haibadiliki wala viongozi wake hawabadiliki.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.