Mbowe, DC Hai ‘jino kwa jino’

Mbowe adai wanaohama wanatekwa na kulazimishwa kujiuzulu, DC agoma kumjibu

Mbowe, DC Hai ‘jino kwa jino’

Mbowe adai wanaohama wanatekwa na kulazimishwa kujiuzulu, DC agoma kumjibu

11 September 2018 Tuesday 10:06
Mbowe, DC Hai ‘jino kwa jino’

Moshi, Tanzania

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameibua tuhuma dhidi ya mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kuwa anakodi vijana wanaoteka viongozi wake na kuwalazimisha kujiuzulu.

Hata hivyo, Sabaya amemjibu Mbowe akisema hawezi kujibizana naye huku katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabhia akisema watazijibu tuhuma hizo kwa uzito wake kwa sababu ni upotoshaji wa kiwango cha juu na hakikubaliki.

Mbowe, ambaye ni mbunge wa Hai alikwenda mbali na kudai baadhi ya walioandika barua za kujiuzulu walifanya hivyo chini ya vitisho.

Mbowe, alidai vijana hao aliowaita wahuni wameingizwa wilayani humo kutoka Arusha na mkuu huyo wa wilaya, wakijifanya ni maofisa usalama, huku wakiwasaka viongozi wa Chadema usiku na mchana.

Alisema kutokana na uzito wa alichodai ni kutekwa kwa viongozi wa chama chake na kulazimishwa kujiuzulu, huku wengine wakitishwa, atalipeleka suala hilo bungeni kwa sababu yeye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Hata hivyo, Sabaya alipozungumza na Mwananchi kuhusu tuhuma hizo, alijibu kwa kifupi kuwa hawezi kujibizana na mtu anayekaribia kuchanganyikiwa bila kutaka kuingia kwa undani.

“Nimejipangia utaratibu wa kutojibizana na mtu anayekaribia kuchanganyikiwa. Sina comments (maoni) zaidi,” alisisitiza mkuu huyo wa wilaya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo za utekaji na matumizi ya silaha, alitaka Mbowe mwenyewe ndiye aulizwe ili athibitishe.

“Muulizeni Mbowe mwenyewe ili athibitishe hicho alichokisema. DC (mkuu wa wilaya) naye ni msimamizi wa sheria na masuala ya usalama, muulizeni na yeye,” alisema Kamanda Issah.

Hata hivyo, katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mabhia alisema wamesikia alichokiita kuwa ni propaganda za Chadema na kwamba watazijibu kwa uzito wake kwa kuwa huo ni upotoshaji wa kiwango cha juu ambacho hakikubaliki.

“Tuliposikia hizo propaganda tangu siku ya kwanza hao wenyeviti 18 walipojiuzulu, tuliwaita mbele ya vyombo vya habari na kuthibitisha kuwa hawakulazimishwa bali walijiuzulu kwa hiari yao,” alisema Mabhia.

Alipoulizwa kuhusu mwenyekiti wa kijiji cha Uraa aliyesimama jukwaani juzi na kudai alishurutishwa kusaini barua hiyo, Mabhia alisema yote hayo watayajibu, hivyo wananchi wawe na subira watapata taarifa sahihi.

Mbowe alitoa tuhuma hizo juzi jioni wakati akizindua mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata ya Machame Uroki uliofanyika katika kitongoji cha Bwani, kijiji cha Uraa.

Katika mkutano huo, mwenyekiti wa kijiji hicho, Seth Munisi ambaye jina lake liko katika orodha ya viongozi wa vijiji 18 waliojiuzulu, alipanda jukwaani kuelezea namna alivyolazimishwa kusaini barua.

Munisi alidai alilazimika kusaini barua hiyo saa 6:00 usiku ili kusalimisha maisha yake baada ya kusimamiwa na kulazimishwa na watu hao ambao hawajui, lakini akasisitiza hajajiuzulu uenyekiti.

Akihutubia mkutano huo uliohudhuriwa pia na wabunge; Susan Kiwanga (Mlimba) na Grace Kiwelu (viti maalumu), Mbowe alidai mbinu hizo hazitaisadia CCM, badala yake zinaongeza chuki kwa jamii.

“Wananchi wamechagua viongozi wao halafu anakuja mkuu wa wilaya eti amekuja kuua Chadema Hai. Namwambia mkuu wa wilaya achana na Mbowe,” alisema Mbowe. “Wilaya ya Hai haitaacha Chadema kwa sababu ya wenyeviti wa vijiji wamelazimishwa kuhama. Itabaki kwa sababu Chadema iko kwenye mioyo ya wananchi. Chadema ni imani.”

Alisema, “analeta vijana wahuni kutoka Arusha wanatembea usiku na mchana wanawinda wenyeviti wa Chadema. Wanawakamata wanawatishia na kuwalazimisha kusaini eti wamehama Chadema kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli. Uongozi gani huu?”

“Eti leo wanaona sifa kusema vijiji 18 havina wenyeviti wakati wamewalazimisha kwa vitisho.”

Alisisitiza kuwa, “hicho kikosi kinajiita ni usalama lakini ni wahuni wameokotwa Arusha, wanaletwa huku na vyombo vya dola vinajua na mkuu wa wilaya anajua na wanakaa kimya.”

“Ninalipeleka bungeni hili tujue kama nchi hii tunaweza kuwageuza wananchi ndondocha. Tuna vijiji 20 havina uongozi eti wamelazimishwa wahame. Huu si uongozi tunaoutaka katika nchi hii. Leo tunachoma Sh300 milioni kurudia uchaguzi wa diwani na tunachoma Sh3 bilioni kurudia uchaguzi wa mbunge, hatuoni kuwa hii ni hasara kwa nchi.”

Mwalimu atumia Biblia, Quran

Akizungumza katika mkutano huo, naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alidai baadhi ya wanachama wanahama kwa sababu ya ulimbukeni uliowatawala.

“Kwa wale wenzangu Wakristo naomba niwatie moyo sana. Nendeni leo (jana) usiku mkirudi nyumbani mkasome Biblia waraka wa kwanza wa Yohana sura ya pili msitari wa 19,” alisema Mwalimu.

Akinukuu mstari huo, alisema, “wanatoka kwetu lakini hawakuwa wa kwetu. Wangelikuwa wa kwetu wangelibaki na sisi ili Mungu awadhihirishe kuwa hawakuwa wa kwao. Hawa wanaotoka hawakuwa wa kwetu ndiyo maana wanatoka ili maneno ya Mungu yatimie.”

“Waislamu sisi tuna aya inasema alama za mtu mnafiki ni tatu. Akiaminiwa haaminiki. Tulikuwa na diwani hapa 2015 tulimwamini tukampa udiwani, leo ameondoka uaminifu wake kwetu.

“Lakini la pili, anasema uongo, haya ni maneno ya Mungu siyo maneno yangu na sio maneno ya Mbowe. Anatuonyesha wanadamu wanafiki wana sura ngapi.”

Alisema, “sura ya tatu ni mtu ambaye akitoa ahadi hatekelezi. Aliyekuwa diwani wa hapa (Robson Kimaro) alituahidi lakini kabla ya kufika 2020 amekimbia. Hata Mungu amewaambia alama za mtu mnafiki.”

Mwalimu aliahidi kupiga kambi katika kata ya Machame Uroki na ile ya Kia hadi siku ya kupiga kura Septemba 16.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.