Mbunge Jaguar yupo Tanzania

Mbunge Jaguar yupo Tanzania

19 July 2019 Friday 04:43
Mbunge Jaguar yupo Tanzania

MBUNGE wa Starehe nchini Kenya Charles Kanyi Jaguar yupo nchini Tanzania ikiwa ni siku chache tu baada ya kutoa matamshi yaliyozua utata .

Kiongozi huyo ambaye picha zake za mtandao wa Instagram zimemuonyesha akiwa mjini Dar es Salaam na Dodoma nchini Tanzania amesisitiza taarifa yake ya awali akisema kwamba alieleweka vibaya kuhusu matamshi aliyotoa kuhusu raia wa kigeni wanaoishi nchini Kenya.

''Mimi nilimaanisha wale wanaofanya biashara haramu nchini Kenya ndio wanaopaswa kufurushwa. Mimi hakuna mahali nilikosea na hakuna nchi inayoweza kuruhusu watu wasio na vibali kuingia na kufanya biashara haramu'', alisema mbunge huyo wa kaunti ya Nairobi

Kiongozi huyo ambaye pia ni msanii wa muziki wa kizazi kipya amesema kwamba yuko nchini Tanzania kwa siku nne kuijulia hali familia yake mbali na kuwatembelea marafiki zake.

''Mimi naipenda Tanzania kwa sababu ni nchi nzuri na kama unavyojua nina kijana huku. Nawaambia Watanzania kwamba nawapenda sana na ndio sababu nimetembea hapa pia kama mtalii ili kuipatia kipato nchi hii'', aliongezea kiongozi huyo.

Msanii huyo wa wimbo wa 'Kigeugeu' amesema kwamba anapanga kukutana na wabunge marafiki zake wa taifa hilo kama vile Profesa J na Sugu pamoja na wasanii tofauti.

Kiongozi huyo alizua utata nchini Tanzania aliponukuliwa katika kanda moja ya video iliosambaa katika mitandao ya kijamii akiwataka raia wa kigeni wanofanya biashara nchi humo kufurushwa.

"Ukiangalia soko zetu, Watanzania na Waganda wamechukua biashara zetu, sasa sisi tumesema enough is enough".

Hatahivyo mbunge huyo alijitokeza tena na kukana madai hayo na kusisitiza kwamba alimaanisha raia wa kigeni walioingia nchini humo kwa njia haramu.
Matamshi hayo yalizua mjadala katika bunge la Tanzania huku waziri mkuu, Kassim Majaliwa akimtaka balozi wa Kenya nchini Tanzania kutoa kauli ya serikali ya kenya

Hatahivyo Kenya ilijitenga na matamshi hayo ikisema yalikuwa ni binafsi

Na licha ya matamshi hayo yaliodaiwa kuwa ya chuki kuzua mjadala mwengine katika bunge la Kenya, huku baadhi ya wabunge wakimuunga mkono mwenzao, kiongozi huyo wa Starehe alikamatwa na kuzuiwa kwa siku kadhaa kabla ya kufikishwa mahakamani ambapo alishtakiwa kwa kufanya uchochezi.

Hatahivyo aliachiliwa kwa dhamana baada ya mawakili wake kuwasilisha ombi hilo.

Lakini mjadala huo hakuishia hapo kwani rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alifunga safari kuelekea nchini Tanzania ambapo alikutana na mwenyeji wake Pombe Magufuli nyumbani kwake huko Chato.
Charles Njagua Kanyi al maarufu Jaguar ni mwanamuziki, mwanasiasa na mjasiliamali na inaaminiwa kuwa mmoja wa wasanii tajiri nchini Kenya na katika eneo la Afrika Mashariki

Alizaliwa katika familia ya maskini katika familia ya watoto watatu. Jaguar alisomea katika shule ya msingi mjini Nairobi na akiwa na umri wa miaka 11 alifiwa na mama yake ambaye wakati huo alikuwa ndiye mlezi wake pekee.

Alilazimika kufanya kazi za vibarua ili kujikimu kimaisha na moja ya kazi alizozifanya ilikuwa ni kazi ya ukondakta wa mabasi ya abiria, maarufu daladala au matatu, na kwa msaada wa marafiki aliweza kumaliza shule.

BBC

Updated: 19.07.2019 06:22
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.