banner68
banner58

Nape aamua kusema la moyoni kuhusu sheria kandamizi nchini

Nape aamua kusema la moyoni kuhusu sheria kandamizi nchini

13 June 2018 Wednesday 12:37
Nape aamua kusema la moyoni kuhusu sheria kandamizi nchini

Na Mwandishi wetu

MALUMBANO baina ya Mbunge wa Mtama (CCM) Nape Nnauye na wafuasi wake kuhusu bao la mkono yameendelea ambapo safari hii ameamua kutoa ya moyoni.

Nape amekubali kulaumiwa kwa kauli yake ya “bao la mkono”, lakini akataka asihusishwe na sakata la kufungiwa kwa mtandao wa kijamii wa Jukwaa la Jamii, maarufu kwa jina la Jamii Forums.

“Hili la JF linafikirisha! ukizuia watu kusema wayawazayo unaweza kukutana nao... kimya kimya,” aliandika Nape katika akaunti yake juzi na kuibua mashambulizi kutoka sehemu tofauti.

Wafuasi walimtaka asijihusishe na masuala ya uhuru wa vyombo vya habari kwa madai kuwa ndiye mwanzilishi wa sheria zinazokandamizi vyombo vya habari.

Akizungumza na waaandishi mjini Dodoma, Nape alisema baada ya watu kuona ameweka ujumbe huo walianza kumshutumu kwa mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kumtuhumu kuwa ndiye aliyehusika kutunga sheria hiyo inayotaka mitandao ya jamii ambayo haijasajiliwa kusitisha usambazaji wa taarifa.

Lakini, Nape aliwajibu kuwa hahusiki na Sheria ya Makosa ya Kimtandao wala kanuni zake zilizosababisha Jamii Forums kufungwa kwa kuwa ilitungwa hata kabla ya yeye kuwa mbunge na baadaye waziri.

“Watu hawakuishia kunituhumu na utunzi wa sheria hii ambayo kiukweli ilipotungwa sikuwa mbunge na wengine ndio wakaja na hili neno bao la mkono,” alisema katibu huyo wa zamani wa itikadi na uenezi wa CCM alipozungumza na Mwananchi jana.

Alisema baada ya kuona upotoshaji kuhusu kauli ya bao la mkono ndipo alipoandika tena kauli hiyo iliyoibua utata wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

“Nilaumuni kwa bao la mkono lakini sio kwa hili la JF’,” Nape ameandika katika akaunti hiyo na kuibua mjadala mwingine.

Nape alitoa kauli hiyo ya “bao la mkono” Juni 22, 2015 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Nyehunge wilayani Sengerema, Mwanza wakati akiwa katika msafara wa katibu mkuu wa zamani wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Kauli hiyo ilitafsiriwa kuwa ni CCM kujiandaa kushinda uchaguzi kwa njia yoyote, hata isiyo halali kutokana na kufananishwa na bao la mkono lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa Argentina, Diego Maradona katika mechi ya soka ya Kombe la Dunia, mchezo ambao wachezaji hawaruhusiwi kutumia mikono isipokuwa kwa makipa tu.

Wakati huo, Nape alilazimika kutoa ufafanuzi kujaribu kuiweka sawa kauli yake katika kipindi ambacho joto la uchaguzi lilikuwa linapanda hivyo kufanya iwe shida kwa wapinzani kumuelewa.

Kadhia hiyo ndiyo imemkumba tena jana baada ya kurudia kauli hiyo ya “bao la mkono” na kulazimika kurudi Twitter kufafanua.

“Naomba turudishe visu vyetu kwenye ala: namaanisha nilaumiwe kwa kuasisi usemi wa ‘bao la mkono’. Simjui na siamini kama kuna aliyefunga bao la mkono mwaka 2015. Mimi mwenyewe nilibanwa Mtama kampeni nzima na kuponea chupuchupu,” ameandika Nape kwenye akaunti yake.

Waliochangia maoni yao ndio walioonyesha kukerwa, wakimtuhumu kuwa alitoa ufafanuzi ili kurekebisha mambo baada ya twiti yake ya kwanza kuonekana kuwa na madhara.

Azania Post

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.