Tundu Lissu: Nafungua kesi dhidi ya Spika Ndugai

Tundu Lissu: Nafungua kesi dhidi ya Spika Ndugai

29 June 2019 Saturday 06:36
Tundu Lissu: Nafungua kesi dhidi ya Spika Ndugai

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam
MWANASIASA  mwandamizi wa upinzani nchini, Tundu  Lissu anapanga kwenda Mahakama Kuu kupinga kuvuliwa ubunge wake.

Anakwenda mahakamani muda mfupi baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, Juni 28, 2019 kulitangazia bunge kuwa ameiandikia tume ya uchaguzi kuileleza kuwa jimbo la Singida Mashariki, lililokuwa likishikiliwa na Lissu kupitia chama kikuu cha upinzani Chadema lipo wazi.

Mwanasiasa huyo pia amesema yeye si mtoro bungeni na yungali anapokea matibabu barani Ulaya.

Spika Ndugai ametaja sababu kuu mbili zilizomsukuma kuiandikia tume ya uchaguzi barua hiyo, mosi ni kutokana na Lissu kutokuhudhuria bungeni kwa muda mrefu na pili kutokuwasilisha fomu ya tamko la mali na madeni kwa sekretari ya maadili kwa mujibu wa sheria.

Lakini Lissu amezipinga hoja zote mbili, akisema hashangazwi na tamko la Spika Ndugai.

"Mimi si mtoro bungeni na sijawahi kuwa mtoro. Kilichonikuta kinajulikana, nilipigwa risasi 16 nikiwa natoka bungeni Septemba 7, nikaletwa nje kwa matibabu. Tangu hapo nipo nje natibiwa," amesema Lissu na kuongeza, "Kwanza walionishambulia mpaka sasa hawajulikani, hakuna aliyekamatwa. Leo inasemwa sijulikani nilipo navuliwa ubunge... kinachoendelea si ajabu, kuna watu hawana maarifa tena, walichobaki nacho ni mabavu tu."

Japo inafahamika kuwa mwanasiasa huyo alilazimika kusafirishwa nje ya Tanzania awali nchini Kenya na kisha Ubelgiji kwa matibabu baada ya shambulizi dhidi yake, kumekuwa na mjadala mkubwa juu ya kutokuwepo kwake bungeni kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Hivi karibuni ikiwa ughaibuni amezuru nchi za Marekani, Ujerumani na Uingereza, kote huko, amehojiwa na vyombo vya habari kwa kutoa mihadhara kwenye vyuo vikuu juu ya hali ya haki za binaadamu Tanzania.

Hali hiyo iliibua hoja miongoni mwa wakosoaji wake kuwa tayari amepona na anastahili kurudi Tanzania.

Spika Ndugai, Februari 2019 alikubali kufanyia kazi hoja ya kuzuia stahiki zake kama mshahara kwa madai hayo, na kusema kuwa hana taarifa rasmi juu ya alipo Lissu na hali yake ya kiafya, na amekuwa akimuona kwenye vyombo vya habari.
Na wakati akitoa taarifa juu ya kuvuliwa ubunge wake Spika Ndugai ameendelea kushikilia msimamo wake kuwa bado hana taarifa rasmi ya alipo Lissu na anachokifanya kwa sasa huko alipo.

"Katiba yetu inasema, katika mazingira yote mawili (kutooneka bungeni bila taarifa rasmi, na kutowasilisha tamko la mali na madeni) ubunge wake unakoma na ataacha kiti chake, ndiyo lugha inayotumika na katiba…kwa hiyo unakuwa umejifuta mwenyewe ubunge, hujafukuzwa na mtu," amesema Spika Ndugai.

Lissu amesema nini hasa?
"Ni aibu kwa Spika wa Bunge kusema hajui nilipo, ilhali dunia nzima inajua nipo Ubelgiji na naendelea na matibabu. Kila siku mimi naenda hospitali kufanya tiba ya mazoezi, siwezi kutembea bila kufanya mazoezi hayo," amesema Lissu na kuongeza; "Ofisi ya bunge inajua fika nilipo. Katibu wa Bunge ameshawahi kuwasiliana kwa barua na kaka yangu kuhusu matibabu yangu na nakala ya barua iliyotumwa na katibu ilinifikia nikiwa hospitali Ubelgiji. Wanajua nilipo."

Lissu amesema kufuatia kauli hiyo ya Spika, anawasiliana na mawakili wake nchini Tanzania ili wamwandikie kuomba nakala ya barua alotuma tume ya uchaguzi na pia kuiomba tume hiyo iwape nakala ya barua kutoka kwa Spika.

Hatua itakayofuata baada ya hapo ni kulifikisha suala hilo Mahakama Kuu.

"Tunaenda Mahakama Kuu ili iseme kama kweli Spika hajui nilipo, na kwa nini sipo Bungeni. Pia iseme kwa mazingira yangu na yaliyonikuta kama jimbo lipo wazi," amesema Lissu.

Lissu anaamini hatua ya Spika imekuja wakati huu kwa sababu ametangaza kuwa atarejea Tanzania mwezi wa tisa.
"Hawa watu wana hofu juu yangu, wana hofu juu ya Septemba 7 siku nitakayorudi Tanzania. Siku ambayo itatimu niaka miwili kamili toka niliposhambuliwa. Hakuna cha kunizuia kurudi," amesisitiza.

Lissu alikuwa miongoni mwa wanansiasa wa upinzani waliopendelea kumuita Magufuli kuwa 'Dikteta Uchwara' ama kwa lugha ya kingereza'Petty Dictator'.

Baada ya shambulio hilo, alikimbizwa Nairobi kwa matibabu kisha Brussels Ubelgiji toka mwezi Januari mwaka 2018.

Huko kote aliendelea kusisitiza kuwa serikali ya Magufuli ilikuwa na mkono kwenye shambulio dhidi yake.

Hata hivyo, katika miezi ya hivi karibuni Lissu ametoka Ubelgiji na kuzuru nchini Uingereza na kufanya mahojiano na runinga ya BBC, Kisha akazuru Ujerumani na kufanya mahojiano na runinga ya DW.

Kote huko, Lissu ambaye ni mbunge kupitia chama cha upinzani cha Chadema ameendelea kusisitiza kuwa serikali ya rais John Magufuli ilikuwa na mkono kwenye shambulio dhidi yake.

Pia amelishambulia Bunge chini Spika Job Ndugai kwa 'kumtelekeza' na kushindwa kulipia matibabu yake nje ya nchi.

Lissu pia amekuwa akilituhumu bunge chini ya Spika Job Ndugai kwa 'kumtelekeza' na kushindwa kulipia matibabu yake nje ya nchi.

Gharama za matibabu
Spika Ndugai aliliambia bunge kuwa si kweli kuwa chombo hicho kimtelekeza Lissu.

Ndugai alidai dai kuwa hadi mwishoni mwa Desemba 2018, Lissu alikuwa amelipwa milioni 207.8  pamoja na milioni 43 zilizotolewa kama mchango wa matibabu yake na wabunge wenziwe na kufanya jumla kuu ya fedha alizolipwa kuwa  milioni 250.

Hata hivyo, Lissu alimjibu Ndugai na kunukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema bunge la Tanzania halijawahi kutoa hata senti moja kugharamia matibabu yake.

Lissu amekiri kulipwa milioni 43  zilizotolewa na wabunge wenzake kama mchango wao na kwamba kiasi kingine alicholipwa kinachofanya jumla ya fedha hizo kufikia Sh250 ni mishahara na stahiki zake, lakini siyo gharama za matibabu.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.
Avatar
Yassin Sadik 2019-06-30 16:23:16

Thanx very much.

Avatar
ndikumana simon 2019-07-06 10:03:13

polesana lissu mungu anakuona jimbo badonilako