Viongozi wa dini wataka wanawake kugombea uchaguzi Serikali za Mitaa

Viongozi wa dini wataka wanawake kugombea uchaguzi Serikali za Mitaa

07 September 2019 Saturday 07:08
Viongozi wa dini wataka wanawake kugombea uchaguzi Serikali za Mitaa

Na Francis Machibya, Dar es Salaam

KAMATI ya viongozi wa Dini mbalimbali nchini, imewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki na kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa ili kushika nafasi mbalimbali za uongozi. Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Novemba 24, 2019.

Wito huo umetolewa hivi karibuni jijini Dar es salaam na Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Charles Kitima katika kilele cha kongamano kuhusu Nafasi ya Mwanamke katika Uongozi wa kuchaguliwa na kwamba wanawake wawe na uthubutu kuchukua fomu na kugombea nafasi katika uchaguzi huo.

Kabla ya kongamano hilo kulitanguliwa na semina ya iliyofanyika katika ofisi za baraza hilo ikilenga kuwajengea uwezo wanawake kujitokeza kugombania nafasi mbalimbali za uongozi.

"Mafunzo haya yamewawezesha akinamama kutambua wajibu wao katika kujitokeza kushiriki kugombea nafasi kwenye chaguzi mbalimbali ikiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu," amesema Kitima

Kitima amesema viongozi wa dini wamejitoa kuheshimu mitazamo ya wanawake kwenye kupambana na changamoto mbalimbali za kimazingira.

Aidha amewataka wanaume kuwatia moyo wanawake wajitokezee kwa wingi kuchukua fomu na kugombea nafasi za uongozi na kwamba itasaidia kuchoche shughuli za kimaendeleo.

Mwenyekiti taifa wa Wanawake wa Kiislam (Bakwata), Hajat Shamimu Khan amesema wanamke ni nguzo katika familia na taifa hivyo ni muhimu kuwania nafasi za uongozi .

"Mafunzo yalikuwa mazuri yametujenga akinamama kuweza kukabiliana na ushindani mkubwa wa kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa," amesema Khan.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Mennonite Dayosisi ya Mashariki Maira Migire amewataka wanawake kuepuka baadhi ya misemo inayowakatisha tamaa badala yake wachangamkie fursa za kuwa viongozi katika jamii inayowazunguka.

Askofu Mkuu wa Katoliki Jimbo la Bukoba Mjini Method Kilaini amewasihi wanawake kuwania nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya kata hadi taifa na kuwasisitiza wakinababa kutowavunja moyo.

Mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) Renatha Selemani amesema matamko ya Shirika la Haki za Binadamu yanatambua usawa kati ya wanawake na wanaume katika nafasi za uongozi na kusisitiza Katiba ya Jamhuri ya Muungano inampa haki mwanamke kushiriki katika nafasi za uongozi

Updated: 07.09.2019 07:20
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.