Tanzania inaagiza asilimia 61 ya malighafi za kutengeneza mabati

Tanzania inaagiza asilimia 61 ya malighafi za kutengeneza mabati

13 August 2018 Monday 23:06
Tanzania inaagiza asilimia 61 ya malighafi za kutengeneza mabati

Tanzania inaagiza kutoka nje asilimia 61 ya malighafi zinazotumika kutengenezea mabati nchini, kikiwa ni  kiwango cha juu zaidi ikilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Kenya wanaagiza malighafi hizo kwa asilimia 15 na Uganda asilimia saba.

Kiwango hicho kinaathiri ukuaji wa viwanda vya ndani kwa sababu bidhaa nyingi zinaagizwa kutoka nje, hivyo zinaongeza ushindani sokoni kwa viwanda vya ndani ambavyo vinatumia gharama kubwa za uzalishaji.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Agosti 13, 2018 Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Alaf Tanzania, Dipti Mohanty katika ziara ya Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Amesema uwezo wa uzalishaji wa bati hapa nchini ni tani 140,000 wakati mahitaji ni tani 150,000 kwa mwaka.

Mohanty amesema changamoto nyingine ni ushindani usiokuwa sawa hasa kutokana na uwepo wa wauzaji wa bidhaa hiyo wanaoagiza kutoka nje, wakilipa kodi kidogo lakini pia kuingiza bidhaa zisizo na ubora.

"Alaf tumefanya uwekezaji wa Sh430 bilioni, tumetengeneza ajira nyingi na tunalipa kodi lakini wapo wenzetu wengine wana uwekezaji mdogo wa Sh1 bilioni lakini bidhaa zao zimejaa sokoni," amesema mkurugenzi huyo.

Mkurugenzi huyo amesema kampuni hiyo inakabiliwa pia na changamoto ya umeme ambao wakati mwingine unatakatika na kusababisha hasara.

Amesema sasa wako kwenye mpango wao wa kutengeneza chanzo cha umeme maalumu kwa ajili ya kiwanda hicho.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Suleiman Saddiq  maarufu Murad ameiagiza Serikali kukaa na wenye viwanda kujadili sababu za uzalishaji wa ndani kuwa ghali kuliko kuagiza bidhaa nje ya nchi.

Murad amesema viwanda vya ndani vinatakiwa kupewa kipaumbele kwa sababu vinazalisha ajira kwa watanzania wengi, hivyo serikali haina budi kukaa na wamiliki wake kubaini changamoto zinazowakwamisha katika uzalishaji.

"Kiwanda hiki kinafanya vizuri katika uzalishaji na tumeona wamefanya uwekezaji mkubwa ambalo lazima ujengewe utaratibu ili uwe na manufaa kwa Watanzania," amesema Murad ambaye pia ni mbunge wa Mvomero.

Amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya viwanda, Biashara na Uwekezaji kulisimamia Shirika la Viwango nchini (TBS) ili liwe na uwezo wa kudhibiti ubora wa bidhaa sokoni.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.